TAMASHA LA MATUMAINI IMEBAKI SIKU MOJA PEKEE


Na Nassor Gallu
SIKU zinahesabika kuelekea tamasha babkubwa na la kihistoria la Usiku wa Matumaini, linalotarajiwa kufanyika keshokutwa Ijumaa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Kikosi cha Bongo muvi.
Kuelekea tamasha hilo, tayari mkali wa ngoma ya Johnny, Yemi Alade kutoka Nigeria, amedondoka jana jijini Dar kwa ajili ya kuwasha moto wa burudani kwa kuachia shoo kali jukwaani kwa kupigwa ‘tafu’ na mastaa kibao kutoka Bongo.
Akizungumza na gazeti hili, mratibu wa tamasha hilo, Luqman Maloto, alisema taratibu zote kuelekea siku hiyo zimeshakamilika na kinachosubiriwa ni shoo kali itakayoongozwa na Alade siku hiyo ya Ijumaa.
“Niwahakikishie tu kwamba, sisi kama waandaaji tayari tumekamilisha taratibu zote ikiwemo utaratibu mzuri ambao utamfanya kila atakayehudhuria uwanjani kuinjoi.
“Mashabiki wa burudani waje kwa wingi kuona shoo kali na burudani nyingine kabambe ambazo ninaamini zitakuwa kivutio na kuweka kumbukumbu katika vichwa vyao,” alijinasibu Maloto.
Katika tamasha hilo litakalofanyika kwa mara ya tatu mfululizo tangu kuanza kwake, safari hii kutakuwa na burudani tofauti ambayo ni pamoja na mechi kali ya wabunge wanaoshabikia Yanga dhidi ya wenzao wa Simba, Bongo Fleva dhidi ya Bongo Movie huku mastaa kibao wa muziki wakiongozwa na Madee, Roma Mkatoliki, Menninah, Navy Kenzo, Scorpion Girls, Nyandu Toz, Juma Nature na kundi zima la TMK Wanaume Halisi na wengine kibao, wakishusha shoo ya kufa mtu.
Masumbwi
Bondia mwenye roho mbaya anayetambulika na Chama cha Ngumi Tanzania (TPBO) ambaye ni bingwa wa zamani wa Afrika Mashariki na Kati, Mada Maugo ‘Maugo Jr’, atapanda ulingoni kuchapana makonde na bondia mwenye ngumi kali anayeshikilia mkanda wa UBO ambaye ni bingwa wa sasa wa Afrika Mashariki na Kati, Thomas Mashali ‘Simba Asiyefugika’.
Mashali na Maugo ni mabondia wenye upinzani mkali ndani na nje ya ulingo, kitu ambacho huongeza chachu ya ushindani katika mpambano huo huku Maugo akiwa na kumbukumbu mbaya ya kukung’utwa katika pambano la mwisho walilokutana wababe hao Agosti 30, 2013, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.
Bongo Movie vs Bongo Fleva
Bonge la mechi litakalowahusisha mastaa kibao wa muziki wa Bongo Fleva kushuka uwanjani kupepetana na wenzao wa Bongo Movie.
Kikosi cha Wabunge.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Bongo Movie, Fatuma Makongoro ‘Bi Mwenda’, alisema kikosi chake kitakuwa na wakali kibao kama Mzee Majuto, Kingwendu, Dk Cheni, Bambo, JB, Steve Nyerere huku Bongo Fleva ikiundwa na Peter Manyika, H-Baba, Ali Kiba, Rich One, Kalapina na wengine.
Yanga vs Simba
Wabunge wa Yanga wakiwa na mwanafamilia mpya, Ridhiwani Kikwete, watashuka dimbani kupepetana na wenzao wanaoshabikia Simba wamaong’ara na straika ‘matata’ Wiliam Mgimwa kutoka Iringa ambao wameahidi kulipiza kisasi.
Ikumbukwe kuwa, katika mchezo waliokutana mwaka jana katika tamasha hili, wabunge wa Simba walitoka kichwa chini baada ya kulambishwa bao 1-0, jambo linalofanya mchezo huu kuwa mgumu na wa upinzani, kwani Simba hawatakubali kuwa wateja kwa mara nyingine.
Baadhi ya wabunge wa Yanga ni Joshua Nassari, Abasi Mtemvu, Mwigulu Nchemba, Ridhiwani Kikwete na Freeman Mbowe na Simba inaundwa na wakali kama Zitto Kabwe, Wiliam Ngeleja, Juma Nkamia, Ismail Rage na Amos Makalla.
Mgeni rasmi
Mgeni rasmi katika tamasha hili, anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohamed Gharib Bilal, ambaye pia atakuwa mwamuzi katika pambano la Simba na Yanga.
Usiku wa Matumaini ni tamasha linalotumika kuwaunganisha Watanzania katika kuendeleza uzalendo huku asilimia 20 ya mapato yake, ikitumika kuchangia mamlaka ya elimu.
Tamasha hili limepangwa kuanza saa mbili na nusu asubuhi na kumalizika usiku mnene ambapo burudani zote hizi utaziona kwa kuchangia kiasi kidogo cha shilingi elfu tano (5,000) tu getini.
Burudani ya Usiku wa Matumaini inaletwa kwenu kwa udhamini wa Vodacom, Clouds FM, Pepsi, E-FM, Azam TV na Times FM.

Comments

Popular posts from this blog

UTAPELI MZITO: WABONGO WALIZWA 'MIKOPO YA OBAMA NA JK KATIKA TAASISI YA Tanzania Loan Society' , RIDHIWANI AKANA KUHUSIKA, NMB YATOA ONYO

AIBU! MKE, MUME WAZICHAPA WAFUNGA MTAA